Ziara ya Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Iringa Chuoni MUCE
📍 16 Mei 2025 | Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE)
Leo tarehe 16 Mei 2025, Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) kimepokea kwa heshima ujio wa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa. Ujumbe huo umeongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Comrade Daud Yassin, ukiwa na lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu inayotekelezwa kupitia Mradi wa Higher Education for Economic Transformation (HEET).
Katika ziara hiyo, wajumbe walitembelea maeneo mbalimbali ya ujenzi na kushuhudia hatua kubwa zilizofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo. Mwenyekiti wa CCM Mkoa alieleza kuridhishwa kwake na kasi, nidhamu, na ubora wa kazi zinazofanyika chuoni hapo. Aidha, alikipongeza Chuo kwa usimamizi madhubuti wa miradi na kutoa shukrani kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya elimu nchini.
Akizungumza mbele ya Kamati hiyo, Rasi wa Chuo, Prof. Method Samwel Semiono, alieleza kuwa Mradi wa HEET ni mradi mkubwa wa kwanza katika historia ya Chuo unaojenga majengo manne makubwa kwa wakati mmoja, ambayo ni: Jengo la Sayansi, Jengo la Elimu Maalum na Teknolojia ya Habari, Jengo la Wanafunzi wenye Mahitaji Maalum, na Maabara ya Fizikia. Aliongeza kuwa Chuo kitaendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi hiyo kwa kuhakikisha inakamilika kwa wakati, kwa ubora unaotakiwa, na kuandaa mikakati ya kuitunza ili iwe na manufaa ya muda mrefu kwa Watanzania wote.
MUCE inajivunia ushirikiano huu wa karibu na Serikali na itaendelea kujikita katika utoaji wa elimu bora na uboreshaji wa mazingira ya kujifunzia na kufundishia.