Ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa Chuoni MUCE
Leo, tarehe 28 Agosti 2025, MUCE ilipata heshima ya kutembelewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, aliyefika Chuoni kuangalia maendeleo ya miradi ya ujenzi wa miundombinu mipya inayotekelezwa na Chuo. Katika ziara hiyo, kabla ya kutembelea miradi ya ujenzi, Mkuu wa Mkoa alipewa taarifa ya safari ya Chuo, mafanikio yake, na mchango wake katika kukuza elimu ya juu nchini.
📖 Safari ya MUCE
MUCE ni sehemu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, iliyoanzishwa mwaka 2005 kwa lengo la kusaidia kukabiliana na uhaba wa walimu wenye shahada katika shule za sekondari. Tangu wakati huo, MUCE imekuwa nguzo muhimu katika sekta ya elimu, na tayari imetoa zaidi ya wahitimu 18,000 waliotapakaa ndani na nje ya nchi.
🎓 Idadi ya Wanafunzi na Mafunzo
Idadi ya wanafunzi imeongezeka kutoka 853 mwaka 2006 hadi zaidi ya 5,900 mwaka 2025. Kwa sasa MUCE inatoa programu 3 za shahada za awali na zaidi ya programu kumi (10) za uzamili, na imeandaa mitaala mipya zaidi ya 28 inayotarajiwa kuanza kufundishwa Mwaka wa Masomo 2026/2027. Lengo la Chuo ni kufikia wanafunzi 6,200 ifikapo 2026 – na tayari MUCE imefikia zaidi ya asilimia 96 ya matarajio hayo.
👩🏫 Idadi ya Watumishi
MUCE kwa sasa ina jumla ya watumishi 440 (279 wanawake na 161 wanaume). Idadi ya wahadhiri wenye shahada ya uzamivu imeongezeka hadi 85, huku maprofesa wakiwa wanne (4) – wakati mmoja (1) miongoni mwao ni zao la MUCE. Ongezeko hili limechangiwa na uwekezaji wa Serikali na kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) ambao umefadhili mafunzo ya watumishi wengi.
🏗️ Uwekezaji katika Miundombinu
Chuo kinatoa shukrani kwa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji mkubwa wa ujenzi wa miundombinu mipya ambayo ni:
• Mabweni ya wanafunzi
• Maabara ya Fizikia
• Jengo la Sayansi
• Jengo la Midia Anuwai na Elimu Maalum.
• Maktaba
Ujenzi huu unatekelezwa kupitia fedha za maendeleo na Mradi wa HEET, wenye thamani ya zaidi ya TZS Bilioni 20.
🙌 Pongezi za Mkuu wa Mkoa
Mhe. Kheri James, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, amekipongeza Chuo kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo, akisisitiza kuwa mpaka sasa hakuna malalamiko kutoka ndani au nje ya Jumuiya ya MUCE ambayo yangeweza kukwamisha utekelezaji wa miradi hiyo. Aidha, alitoa rai kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati kulingana na masharti ya mikataba ya ujenzi, ili wanafunzi na jamii kwa ujumla waanze kunufaika mapema na uwekezaji huo mkubwa wa Serikali.
⚠️ Changamoto na Mikakati
Licha ya mafanikio haya, MUCE inakabiliana na changamoto ya ukosefu wa shule ya mfano ya mazoezi kwa walimu tarajali. Ili kutatua changamoto hii, MUCE imepanga kuanzisha Day Care Centre ifikapo mwaka 2026 – kama mwanzo wa shule ya mazoezi.
MUCE inaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Serikali ya Mkoa wa Iringa na wadau wote wa maendeleo kwa uwekezaji, msaada na ushirikiano wa karibu.
Kwa pamoja, tunajenga chuo imara, chenye dira ya kimataifa, na chenye mchango mkubwa katika maendeleo ya elimu na uchumi wa taifa.