MUCE Yafanya Kikao cha Kwanza cha Mradi wa HEET
Leo tarehe 16 Oktoba 2024, Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) kimefanya kikao cha kwanza (kick off Meeting) cha Mradi wa Elimu ya Juu ya Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) kilichowakutanisha Chuo, kama Mteja (client), Mkandarasi, na Mshauri Mwelekezi wa Mradi wa HEET. Lengo kuu la kikao hicho ni kupata mwelekezo wa utekelezaji wa mradi mzima kwenye ujenzi wa majengo. MUCE, kupitia Mradi wa HEET, inajenga majengo manne: Hosteli ya Wanafunzi, Maabara ya Fizikia, Jengo la Midi Anuai na Elimu Maalum pamoja na Jengo la Sayansi.
Akizungumza kwa niaba ya Rasi katika kikao hicho, Dr. Orestes Kapinga, Kaimu Naibu Rasi - Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu na Msaidizi wa Mratibu wa Mradi wa HEET-MUCE, amesema:
“Tumepita katika maeneo (sites) ambayo ujenzi unaendelea ili kuona kazi ambazo zimekwisha kuanza kufanyika na zile ambazo zinatarajiwa kuanza kufanyika hivi karibuni, na msisitizo umekua ni kuhakikisha mkandarasi anakamilisha mradi huu ndani ya muda muafaka lakini kwa kuzingatia ubora kama ambavyo benki ya dunia wametaka tusimamie”
Kwa upande wake Bw. Dickson Mwaipopo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Dimetoklasa Real Hope LTD, ambaye pia ni Mkandarasi wa Ujenzi wa Majengo ya HEET, ameeleza kufurahishwa na kikao kilichofanyika leo hii kwa sababu kimesaidiana kuwakutanisha kwa pamoja wakishadau muhimu wa ujenzi wa majengo ya HEET, hapa MUCE kujadili kwa pamoja na kupanga vizuri namna njema ya kutekeleza ujenzi wa majengo hayo.
Naye Injinia Dausen Edwin Temu, kutoka Kampuni ya Mekon Arch Consultancy, ambaye pia ni Mshauri Mwelekezi kwenye mradi huu, amesema kikao cha leo kimesaidia wao kufahamu vitu muhimu vya kuzingatia wakati mradi unaanza ili kuweza kuendana na kile kinachotakiwa katika mkataba.
Mradi wa HEET punde utakapokamilika utakuwa umekisaidia Chuo kupiga hatua kubwa kutekeleza malengo ya msingi, ambayo ni kufundish, kufanya utafiti na kutoa huduma kwa jamii, na kusaidia kuandaa wataalam kwenye maeneo mbalimbali, watakaolisaidia taifa kupiga hatua za kimaendeleo.