Skip to main content
MUCE YASAINI MKATABA WA MAKUBALIANO NA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA (BMH) KWA HUDUMA ZA MATIBABU YA HARAKA

MUCE YASAINI MKATABA WA MAKUBALIANO NA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA (BMH) KWA HUDUMA ZA MATIBABU YA HARAKA

Chuo Kishiriki cha Elimu cha Mkwawa kimesaini Mkataba wa Makubaliano (MoU) na Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kwa ajili ya utoaji wa huduma za matibabu ya haraka kwa wafanyakazi wa Chuo. Hafla ya utiaji saini wa mkataba huo imefanyika tarehe 13 Januari 2025.

Mkataba huo umesainiwa na Rasi wa Chuo, Profesa Method S. Semiono, na Profesa Abel Makubi, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Prof. Abel Makubi amesisitiza kuwa kuboresha huduma za afya ni ajenda namba moja ya Hospitali ya Benjamin Mkapa. Ameihakikishia MUCE kuwa hospitali hiyo iko tayari kutoa huduma bora na stahiki kwa wafanyakazi wa Chuo. Aidha, amewakaribisha wafanyakazi wa MUCE kutumia miundombinu ya kisasa iliyopo Hospital ya Benjamin Mkapa, si tu kwa matibabu bali pia kwa uchunguzi wa afya wa mara kwa mara.

Prof. Makubi pia ameonesha utayari wa hospitali kutoa elimu ya afya kwa watumishi wa Chuo ili kusaidia kuwa na wafanyakazi wenye afya njema, kupunguza vifo vya mapema (pre-mature deaths) na kuongeza ufanisi katika kuwahudumia wananchi na Serikali kwa ujumla.

Kwa upande wake, Rais wa Chuo, Prof. Method S. Semiono, ametoa shukrani za dhati kwa uongozi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa mapokezi mazuri na utayari wao wa kusaini mkataba huo. Baada ya shukrani, Prof. Semiono alitoa maelezo mafupi kuhusu Chuo, huduma zake pamoja na idadi ya wafanyakazi na wanafunzi.

Akizungumzia umuhimu wa mkataba huo, Prof. Semiono amesema kuwa ni miongoni mwa mikakati ya Chuo ya kuhakikisha watumishi wanakuwa na afya njema na wanapata huduma za matibabu kwa haraka, jambo ambalo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Chuo.

Katika hafla hiyo, Prof. Semiono pia aliwasilisha maombi ya ushirikiano zaidi kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa, yakiwemo:

* Kutoa mafunzo ya afya kwa wafanyakazi na wanafunzi wa Chuo pamoja na watumishi wa Kituo cha Afya cha MUCE;
* Ushirikiano katika uandishi wa miradi ya pamoja na tafiti za kisayansi kupitia Kitivo cha Sayansi cha Chuo.

Mkataba huu unatarajiwa kuimarisha ustawi wa afya kwa jumuiya ya Chuo na kukuza ushirikiano wa kitaaluma na kitaalamu kati ya MUCE na Hospitali ya Benjamin Mkapa.

News Order
5