Ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa Chuoni Mkwawa kuelekea Ufunguzi wa Vyuo Vikuu – 17 Novemba 2025
Ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa Chuoni Mkwawa kuelekea Ufunguzi wa Vyuo Vikuu – 17 Novemba 2025
Tarehe 13 Novemba 2025, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, amefanya ziara rasmi katika Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) kujadili maandalizi ya Chuo kuelekea kufunguliwa kwa Vyuo Vikuu nchini tarehe 17 Novemba 2025.
Usalama na Maandalizi ya Mapokezi
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa amejionea maandalizi mazuri yaliyofanywa na uongozi wa chuo, ikiwemo:
• Kuimarishwa kwa usalama ndani na nje ya chuo kupitia kuundwa kwa timu maalum ya usalama.
• Kuunda timu itakayoratibu upokeaji na kuwaongoza wanafunzi pindi watakapowasili.
• Ushirikiano na viongozi wa mitaa ambako baadhi ya wanafunzi wataishi ili kuhakikisha ustawi na usalama wao unaimarishwa hata nje ya maeneo ya chuo.
Tathmini ya Mkuu wa Mkoa
Mhe. Mkuu wa Mkoa alieleza kuridhishwa kwake na kiwango cha maandalizi, hususan katika maeneo ya:
• Usalama
• Huduma za kijamii na kitaaluma
• Mifumo na taratibu za usajili
• Miundombinu na maandalizi ya utoaji huduma kwa wanafunzi wapya na wanaoendelea
Aidha, aliwatakia wanafunzi wote heri na maandalizi mema wanapojiandaa kurejea chuoni kwa muhula mpya wa masomo.
Ujumbe kwa Wanafunzi
Chuo kinawakaribisha wanafunzi wote kwa moyo mkunjufu na kinapenda kuwahakikishia kuwa maandalizi yote muhimu yamekamilika. Huduma zitatolewa kwa viwango vya juu ikiwa ni pamoja na usalama, usajili, maeneo ya malazi, na huduma za kijamii.
Karibuni MUCE – Karibuni Iringa